Mtandao wa Waandishi wa Habari wa Palestina ulisema jana Jumapili kwamba, utawala wa Israel unaendelea na sera yake ya kimfumo ya kuwalenga na kuwaua waandishi wa habari ili kuzuia kuakisiwa kwa ukweli jinai zake za kivita.
Jumuiya hiyo imesema kuna angalau waandishi wa habari wanawake thelathini kati ya wale waliouawa na vikosi vya Israel, na mmoja ambaye aliuawa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Imebainisha kuwa, vikosi vya utawala huo pandikizi pia vinalenga familia za waandishi wa habari wa Palestina, na wameua zaidi ya watu 680 wa familia hizo hadi sasa. Israel pia imekuwa ikilenga taasisi za vyombo vya habari katika vita vyake vya maangamizi, na kuharibu taasisi 115 huko Gaza.
Mapema jana Jumapili, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas ilisema mashambulizi ya hivi punde zaidi ya "makusudi" ya Israel dhidi ya waandishi wa habari wa Palestina ni sehemu ya "mateso na mauaji" yanayoendelea dhidi ya wanahabari.
Takriban waandishi wa habari watano zaidi wa Kipalestina waliuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel huko Gaza, huku utawala huo ukiendelea kulenga vyombo vya habari vinavyoripoti uhalifu wake katika ukanda huo. Hamas imewataja waandishi wa habari waliouawa kuwa ni Aziz al-Hajjar, Nour Qandil, Abdul Rahman al-Abadlah, Khaled Abu Seif, na Ahmed al-Zinati.
342/
Your Comment